Fursa mbalimbali za uwekezaji zimeendelea kuibuka ndani ya Kongani ya Viwanda ya Kwala (KIP) baada ya kuanzishwa kwa kiwanda kikubwa zaidi barani Afrika cha kutengeneza vifaa vya kuzalisha umeme jua (solar power panels), hatua inayotajwa kuinua mauzo ya Tanzania kwenda Marekani mara tatu zaidi ya kiwango cha sasa na kuongeza uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 2 katika muda mfupi.

Kiwanda hicho, kinachomilikiwa na kampuni ya Tanzol, tayari kimekamilika na kimeonekana kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda nchini, huku serikali ikikitaja kuwa “historia mpya ya uchumi wa viwanda Tanzania”. Kiwanda hicho chenye mitambo ya kisasa inayojioendesha kwa hali ya juu, kinatajwa kuwa kikubwa kuliko vyote barani Afrika vinavyozalisha vifaa vya umeme jua.

Akizungumza katika ziara za viongozi wa wizara tano za kisekta katika Kongani ya Viwanda ya Kwala wilayani Kibaha leo Jumatano Desemba 10, 2025, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho zitapelekwa moja kwa moja katika soko la Marekani.

Amesema Tanzol imewekeza dola milioni 300 (sawa na shilingi bilioni 725) katika awamu ya kwanza, na kuanzia mwakani itaanza kuwekeza dola milioni 500 zaidi (takriban trilioni 1.25), hivyo kufanya jumla ya uwekezaji wake kufikia shilingi trilioni 2 katika kongani hiyo pekee.

Aidha, Prof. Mkumbo amesema fursa nyingine muhimu iliyoibuka ni kuanzishwa kwa kiwanda cha kuchakata chuma, ambacho kitakuwa cha kwanza nchini na kitachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa chuma kutoka nje. Kiwanda hicho kinachowekezwa na kampuni mpya kinaanza kwa uwekezaji wa dola milioni 50 (takriban shilingi bilioni 125).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KIP, Janson Haung, amesema pamoja na hatua kubwa zilizopigwa katika eneo la kongani hiyo, mahitaji ya miundombinu ni makubwa zaidi, hasa umeme wa megawati 50 kwa kiwanda cha ‘solar panels pekee, na matumizi ya maji zaidi ya cubic meters 5,000 kwa siku.

Amesema kukamilika kwa kongani hiyo kutazalisha ajira 100,000 moja kwa moja na ajira 500,000 zisizo za moja kwa moja, na kwamba lengo ni kufanya Kwala kuwa kongani bora zaidi Afrika.